ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 15, 2017

HUYU HAPA BINTI ALIYEONGOZA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA.

Sophia Juma, mwanafunzi wa St Marry’s Mazinde Juu ya Tanga ameibuka kidedea katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa leo Jumamosi, Julai 15, akishika namba moja kitaifa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde imeeleza kuwa nafasi ya pili imeshikwa pia na msichana, Agatha Julius Ninga wa Tabora Girls. Wote walikuwa wakichukua masomo ya mchepuo wa Sayansi (PCB).

Kadhalika taarifa hiyo imeeleza kuwa wasichana wameongoza kwa ufaulu ambapo kati ya wasichana 28,731 (38 asilimia) waliofanya mtihani, waliofaulu ni 27,577 (sawa na asilimia 97.21).

Jumla ya watahiniwa 75, 116, walifanya mtihani huo Mei mwaka huu.

 Kwa upande wa watahiniwa wavulana, waliofaulu walikuwa ni 42,975 (sawa na asilimia 95.34) kati ya 46,385.

“Mchanganuo wa ufaulu katika madaraja unaonyesha kuwa watahiniwa walipata daraja la 1-11  umepanda  kwa asilimia 0.59 kutoka asilimia 93.13 mwaka 2016 hadi 93.72 mwaka huu,” imesema taarifa hiyo na kuongeza;

“Pia ufaulu katika madaraja kwa upande wa wasichana umepanda ikilinganishwa na wavulana. Ubora wa ufaulu kwa wasichana ni asilimia 94.07 ikilinganishwa na asilimia 93.49 ya wavulana.”

Shule zilizoongoza

Katika matokeo hayo, Shule ya Wasichana ya Feza Girls ya Dar es Salaam imeibuka kinara kwa watahiniwa wake 67 kufaulu kwa kupata daraja la kwanza na la pili.

Shule nyingine zilizoibuka kidedea katika matokeo hayo ni Marian Boys (Pwani) iliyoshika nafasi ya pili, Kisimiri (Arusha) imeshika nafasi ya tatu na Ahmes (Pwani) imeshika nafasi ya nne.

Shule nyingine  ni  Marian  Girls (Pwani) iliyoshika nafasi ya tano, Mzumbe (Morogoro) nafasi ya sita, St Marry Mazinde Juu (Tanga) nafasi ya saba, Tabora Boys (Tabora) nafasi ya nane, Feza Boys (Dar es Salaam) nafasi ya tisa na Kibaha ya Pwani iliyoshika namba kumi.

Shule zilizoshika mkia

Shule zilizoshika mkia ni Kiembesamaki ya Unguja, Hagafilo (Njombe), Chasasa (Pemba), Mwenyeheri Anuarite (Dar es Salaam) na Ben Bella (Unguja). Nyingine zilizotajwa kushika mkia ni Meta (Mbeya) na Mlima Mbeya (Mbeya).

Nyingine ni Shule ya Sekondari ya Al-Ihsan Girls (Unguja) na St Vicent(Tabora).

Waliofutiwa matokeo

Kadhalika taarifa ya Necta imeeleza kuwa watahiniwa 10 walifutiwa matokeo kwa makosa ya kufanya udanganyifu.

Taarifa ya Dk Msonde imeeleza kuwa kati ya watahiniwa hao kumi, saba ni wa shule na watatu ni wa kujitegemea.

Pamoja na hao kumi, watahiniwa wengine 15 hawakufanya mitihani ya baadhi ya masomo kutokana na  matatizo mbalimbali ikiwamo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya mitihani hiyo.

‘Watahiniwa hao wamepewa fursa ya kufanya mitihani ya kidato cha sita, Mei 2018 kama watahiniwa wa shule,” imesema taarifa ya Dk Msonde.

Pia, wapo watahiniwa 69 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani yote yote, wamepewa fursa ya kufanya mitihani hiyo, Mei 2018.



TOVUTI YA BARAZA LA MITIHANI TANZANIA (NECTA)


MATOKEO KIDATO CHA SITA (ACSEE) 2017


MATOKEO YA DIPLOMA YA UALIMU (DSEE) 2017


MATOKEO YA CHETI CHA UALIMU (GATCE) 2017

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.