ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, October 29, 2016

RAIS MAGUFULI ATIMIZA MIAKA 57 AWASHUKURU WANANCHI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli leo Oktoba 29, 2016 anasherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ambapo anatimiza miaka 57.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa ‘twitter’  Rais Dkt. Magufuli amewashukuru watanzania wote kwa kumtakia heri na kuahidi kuendelea  kuchapa kazi kwa maslahi ya taifa.

“Ninamshukuru Mungu kufikia siku yangu ya kuzaliwa,ninawashukuru watanzania nyote kwa kuniombea , nitafanya kazi kwa moyo na nguvu zangu zote” Amesema Rais Dkt. Magufuli.

Aidha Rais Dkt. Magufuli anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ikiwa anakaribia kutimiza mwaka mmoja tangu alipoapa kuliongoza taifa la Tanzania Novemba 5, 2015.

Rais  Dkt. Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 katika Wilaya ya Chato ambayo ni mojawapo ya wilaya tano za mkoa mpya wa Geita uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Wilaya ya Chato ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na ni mwaka 2012 tu ndipo ilipohamishiwa Mkoa wa Geita.

Friday, October 28, 2016

EXCLUSIVE DJ KFLIP AITEMA LAKE FM ARUDI JEMBE.

Katika picha ya pamoja ni Deejay K-Flip (katikati) baada ya kusaini mkataba mpya na Jembe Fm 93.7 mapema leo baada ya kurejea akitokea redio Lake Fm, wengine katika picha Kushoto ni Meneja wa Vipindi Jembe Fm Mbaba Vc na Eddie Jembe (kulia). 
NA. MWANDISHI WETU.
Dj machachari mwenye maskani yake Kanda ya ziwa toka jiji la miamba Mwanza Deejay K-flip hatimaye leo ijumaa ya tarehe 29 October 2016 ameikacha rasmi redio aliyokimbilia miezi mitatu iliyopita Lake Fm na kusaini mkataba mnono wa kuitumikia redio yake ya awali Jembe Fm.

Huu ni mrejeo wa kushitua sana na inatajwa kuwa ni kama fimbo kali ya maumivu itakayoigharimu radio aliyoikacha kwani baada ya Dj huyo kujiunga nayo miezi kadhaa iliyopita alikuwa ni mmoja wa wachoraji ramani wa redio hiyo kuhusu nini kinatakiwa kwenye soko la ushindani wa sasa.

"Najua hili ni pigo kwao, lakini nawasihi watulie kwani maisha lazima yaendelee, kupanga ni kuchagua nami nimechagua kurudi nilikotoka nyumbani kwetu" alisema K-Flip 


K-Flip na Dj Scopion.
Akizungumzia kuhusu sababu zilizo mfanya kurejea Jembe Fm K-Flip amesema kuwa ndani ya wiki mbili tu za mwanzo baada ya kujiunga na Lake Fm aliona  mzigo mkubwa aliojitwisha, kwani ilimlazimu kujifunza kwa haraka utamaduni mpya wa utengenezaji na uendeshaji vipindi na akawa na wakati mgumu kwani ilimlazimu kugeuka kuwa mwalimu kuwafundisha watangazaji wa kituo hicho mfumo utakao uza redio kwa raia.

"Nakumbuka jinsi nilivyokuwa na wakati mgumu kukipitia kila kipindi na kukisahihisha kwa kuwasilishia maoni yake na marekebisho, ni kazi kweli kwani ilinipasa kuamka mapema kusikiliza kila kipindi na contents zake, kazi ambayo ili nimaliza akili" alisema 


K-Flip na producer Oxy.



"Hapa Jembe Fm watangazaji na Ma-Dj wote wanajua majukumu yao, kila kipindi kimeshiba, ubunifu kila kunapokucha na matirio mpya kila siku, Dj unafanya kazi yako umerelux kiasi kwamba unaweza kwenda hata likizo ukaacha mambo yanaendelea bila wasiwasi, thanx God nimerudi nyumbani najisikia niko mahali sahihi na salama" 

"Pamoja na kwamba niliondoka na kwakuwa sikuondoka kwa ubaya bado nilikuwa nakutana na watu wangu wa nyumbani ambao tuliendelea kula pamoja, kunywa pamoja na kushea burudani mbalimbali pamoja lakini nilikuwa nahisi kuna kitu kama kinapungua hivi, kweli niliteseka na mwisho wa siku nikaamua kuutua mzigo" kisha akaongeza.

"Naomba samahani kwa wale watakao nifikiria vibaya lakini haya ni maisha yangu"

Uamuzi huo umepokelewa kwa shangwe na memba wa redio hiyo


K-Flip na Chriss The Dj.
K-Flip na mtangazi Johari Ngassa.


K-Flip na Bob White Pamba.
Head of Djz wa Jembe DjZ wakuitwa Dj Mike beatz (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Dj K-Flip.
Mengi yalisikika kwenye kipindi cha Hotzone.


CCM YATOA TAMKO JUU YA TAARIFA HASI ZILIZOZAGAA KWA SERIKALI YA MAGUFULI.

Inline image 1
Christopher Ole Sendeka, Msemaji wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo tarehe 28/10/2016 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari,

Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeli, kudhihaki, kukatisha tamaa, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania. 

Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu. 

Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni Watanzania. Je ni tamaa ya madaraka tu au mengine? Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema kwa nchi. 

Ndugu wanahabari,
Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita ya tathmini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Katika taarifa yake hiyo, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.

Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?
-          Tulishuhudia akiwa mgombea urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendera huku katiba na kanuni ya chama hicho  ikivunjwa.  Kidemokrasia, anayepewa fursa ya kupeperusha bendera ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chama hicho. Mgombea ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.

-          Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.

-          CHADEMA watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi  kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalum ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea/mwanachama huyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalum ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia.
Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathmini, kujikosoa, kujisahihisha na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao.

Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewa kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo. 

Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujijenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi.

Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kufanikisha mpango huo.

Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameendela kufanya juhudi kubwa katika kuijenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.

Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya kwa kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari  na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tamaa kwa maslahi ya wachache, ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono katika dhamira yake safi ya kuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na;-
                                                CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016.

VIJANA WA HALMASHAURI YA MSALALA WALALAMIKIA MGODI.

NA ANNASTAZIA MAGINGA, Mwanza

WAKAZI wa kijiji cha Kakola na Bushing'we wa Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, wamelalamikia Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu kutotoa ajira kwao na badala yake kuwapatia wageni ajira ambazo hata wao wanaweza kuzifanya.

Hayo yamebainishwa na wakazi hao wakati wa ziara ya kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na uwekezaji wa migodi ili kuimarisha na kutetea demokrasia na uwajibikaji bora katika sekta ya madini iliyoratibiwa na shirika la Action for Democracy and Local Government (ADLG).

Wakizungunza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi hususan vijana waliohojiwa wamesema kuwa licha ya kuwepo kwa kazi ambazo wanamudu kuzifanya katika mgodi huo, lakini wamekuwa wakinyimwa na badala yake wakipewa wageni kutoka nje ya kijiji chao na kupewa ajira hizo.

Malimi Mbulya amesema vijana ambao ni wakazi wa kijiji Kakola wamekuwa wakiambulia ajira za ulinzi tu kwa kisingizio kuwa hawana elimu wakati wanatambua kuwepo kwa kazi ndani ya mgodi ambazo haziitaji elimu ya juu na wamekuwa wakipewa wageni wan je ya wilaya yao ambao pia hawana elimu kubwa kama wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa huduma za jamii kijiji cha Kakola, Muhidini Ibrahimu, amesema mgodi huo umekuwa ukitoa ajira za sungu sungu ambazo hufanywa kwenye mazingira magumu na kwamba hulipwa Sh 150,000 kwa mwezi na kudai fedha hiyo haiwezi kukidhi mahitaji ya muhusika hasa ikizingatia ugumu wa kazi yenyewe.

Naye Apton Mshobozi ambaye amewahi kufanya kazi katika mgodi huo anasema licha ya kutoa ajira kwake kama mkazi wa kijiji hicho na kutumikia kwa muda wa miaka 10, aliachishwa kazi baada ya kupata ugonjwa wa ngozi kutokana na kemikali za sumu akiwa kazini bila ya kulipwa stahiki zake.

"Nilipata ugonjwa wa ngozi  mwaka 2007 sikuwa peke yangu maana tulikuwa kama wafanyakazi tisa, lakini hakuna ambacho nimekipata kutoka Acacia, walinipeleka kwenye hospitali yao kwa uchunguzi baada ya hapo walinitelekeza hapa kijijini bila hata ya fedha za kununulia dawa za kutibu ngozi hivyo naiomba serikali itusaidie" amesema Mshobozi.

Aidha mtandao huu ulihojiana na Katibu wa Chama cha Wafanyakzi wa Tasnia ya Nishati na Madini (NUMET) Kanda ya Ziwa, Yusuph Kalyango ambaye pia ni Afisa Afya, Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) Taifa amesema sheria ya kazi ya mwaka 2006 (6) na kanuni zake, zinawabana wafanyakazi wa migodini wanapokuwa wakidai haki zao.

"Sheria zetu za wafanyazi wa migodini bado zinatubana kwa sababu mwajiriwa anaeleza anachokilalamikia na mwajili anasema anachokukatalia kwa hiyo kunakuwa na mgongano hii inawapa mwanya kutowalipa na hapa ninachokiona sidhani kama kuna uelekeo wa watu hawa kulipwa stahiki zao kwa sababu anaewachunguza kiafya ni daktari wa Acacia hivyo hawezi kusema ukweli, sio rahisi itabaki kuzungushana tu,” amesema Kalyango.

Hata hivyo licha ya sheria na kanuni kuwabana lakink numet iko tayarikuwasaidia na kwamba wanachokifanya ni mwajili kuwatambua watu hao kuwa walikuwa wafanyakazi wake ili aweze kuwalipa stahiki zao.

SERIKALI YAMLIZA SUMAYE, HAKIMU ATISHIA KUFUTA KESI YA VIGOGO NIDA, UFAULU JUU SIRI NZITO YAFICHUKA.


Hakimu atishia kufuta kesi ya vigogo NIDA, Ufaulu juu siri nzito yafichuka, Serikali yamliza Sumaye, Agizo la JPM kwa wamachinga layeyusha mabilioni Dar. 


 Shule Shinyanga yavunja rekodi, Vita ya CUF na Jecha yatimiza mwaka, Sangoma na mkwe wake kunyongwa kwa mauaji ya albino. 

Wamachinga radhi kupigwa mabomu amri ya Makonda, Serikali yachukua shamba la Sumaye, Ripoti ya mkataba wa Lugumi polisi yafika kwa Ndugai. 

Thursday, October 27, 2016

TIMU YA AZAM FC YAJIFUA KWENYE UWANJA WA KAITABA LEO, KESHO KUPAMBANA NA KAGERA SUGAR VPL.

Wachezaji wa Timu ya Azam Fc wakiwa uwanjani Kaitaba hii leo jioni wakijifua, Tayari kwa mchezo wao na Wenyeji wao Kagera Sugar.
Kipa wa Timu ya Azam FC "Wanalambalamba", Aeshi Manula akiwa na Mwalimu wake.



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu 2016/17, raundi ya 12 inaendelea keshokwa michezo sita ambako mabingwa watetezi Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani Kagera.
Jijini Dar es Salaam, katika Uwanja wa Uhuru African Lyon itakuwa mwenyeji wa Mbeya City ya Mbeya ilihali Mwadui ya Shinyanga itasafiri hadi Mtwara kucheza na Ndanda Fc kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Stand United itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye mchezo utaofanyika Uwanja wa Manungu, ulioko Turiani – Mvomero.
Majimaji itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Majimaji huko Songea. Michezo yote mitano hapo juu itaanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki lakini mchezo kati ya Azam FC na JKT Ruvu itaanza saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam huko Chamazi-Mbagala Dar es Salaam.

BEKI mahiri wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe Baada ya kukosa mechi kama sita alionekana kama bado anaugulia jeraha lililomfanya afanye mazoezi mepesi na akiwa peke yake katika Uwanja wa Kaitaba leo. Jumapili itakuwa ni zamu ya kinara wa ligi hiyo, Simba ambayo itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Tanzania Prisons itapambana na Mbao FC kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Michezo yote ya Dar es Salaam, mfumo wa kuingia utabaki kuwa ni uleule wa kutumia kadi za Selcom kununua tiketi za kielekroniki. Viingilio kwenye mechi za Uwanja wa Uhuru ni Sh 30,000 kwa Jukwaa Kuu (VIP-A), VIP-B na C Sh 20,000 na mzunguko ni Sh 5,000 wakati Kiingilio Uwanja wa Azam ni Sh 10,000 kwa VIP na Mzunguko ni Sh 3,000.


Kipa wa Azam Fc


Mashabiki jukwaa kuu wakiwachabo Wachezaji wa Azam Fc kwenye Uwanja wa Kaitaba hii leo


Wakimsikiliza kwa Makini Kocha wao

Shabiki mkubwa na Mpenzi wa Timu ya Azam Fc Ally Kulialia nae alikuwepo Uwanjani hapo



Mwalimu wa Makipa(kulia) wa Azam Fc

Kipa wa Timu ya Azam FC "Wanalambalamba", Aeshi Manula