ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 10, 2015

AHADI ZA MARAIS MKAPA (MSTAAFU) NA DK. KIKWETE HAZIJATEKELEZWA

 NA PETER FABIAN, MAGU. 

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza (CCM), Miraji Mtaturu, ameitaka serikali kupita Wizara ya Maji kutekeleza haraka kwa vitendo, ahadi za Marais wa awamu ya tatu na nne ya kumaliza tatizo la maji na kuwapatia wananchi maji safi na salama wa Mji wa Magu Mkoani Mwanza. 
Mtaturu alisema kuwa Chama Tawala ‘kinalilia’ ahadi hiyo ambayo awali ilitolewa na Rais Benjamin Mkapa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 1995 katika uwanja wa Sabasaba mjini hapa na Rais Dk Jakaya Kikwete mwaka juzi kwenye uwanja huo huo. 

Katibu huyo alisema kwamba kilio cha wananchi walichokitoa katika mkutano wa hadhara Aprili 2 mwaka huu kinaonyesha Wizara ya Maji bado inasuasua kumwajibisha Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo, hivyo viongozi wa juu wa Serikali na Wizara wambane na kumuwajibisha Mkandarasi mshauri wa maradi huo ambaye ni Kampuni ya MS COWI (T) Ltd ya nchini Denmark. 
Mtaturu akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Magui kwenye uwanja huo wa Sabasaba, Mtaturu alisema kazi ya serikali ni pamoja na kutekeleza ahadi ya Rais ambayo kimsingi ni agizo hivyo anashangazwa na kutotekelezwa haraka kwa mradi wa maji safi na salama kutoka katika chanzo cha ziwa Victoria, ulioahidiwa na marais hao.
 “Serikali inataraji kutumia kiasi cha fedha Euro milioni 5.3 zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Magu na vijiji jirani lakini cha kushangaza kila mara Mkandarasi msanifu huyo amekuwa akitoa taarifa za kuendelea na upembuzi yakinifu, upembuzi hadi lini watu wanataka maji,” alisema Katibu huyo na kushangiliwa na umati wa wananchi.

 Aidha alieleza kuwa, Mkandarasi huyo anaonekana kuwa tatizo kwani wakati wa ziara zake wilayani Ukerewe na Sengerema, MS COWI (T) Ltd imeelezwa kuwa tatizo la kuchelewesha baadhi ya miradi ya maji na kila wataalamu wa maji wanapoulizwa wanatoa majibu ya danadana na yasiyo ya kulidhisha. 
“Mkandarasi huyu amezidiwa na kazi Wizara imbane na ikiwezekana imuwajibishe na kumnyima kazi sehemu nyingine, tunaiomba serikali kupitia Wizara kuanzia mwezi ujao (Mei) awe amemaliza Mkandarasi huyo wa usanifu wa mradi ili kazi ya ujenzi wa kuwawekea maji wananchi wa mji huu ikamilike,” alieleza.

 Awali akitoa taarifa kwa Katibu huyo, Mhandisi wa Maji wa Halmasha ya wilaya ya Magu, Joseph Bundala, alisema serikali imeingia mkataba na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EID) kujenga upya mradi wa maji wa mji huo ambao baada ya usanifu mzabubuni atatafutwa kuanza ujenzi. 

Bundala alisema ili kutatua kero hiyo kwa muda, Halmashauri ya wilaya yake imenunua pampu mpya na kufungwa katika chanzo cha maji cha Busulwa ambacho kwa sasa kinatoa huduma hiyo ambayo haijatosheleza kutokana na uchakvu wa miundombinu ya maji kuwa ya zamani. 
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Paul Ntinika alisemakwa kushirikiana na wadau mbalimbali, halmashauri yake tayari imeisha chimba visima 18 na kufunga pampu za mkono katika maeneo ya Magu mjini (visima 6), Ilungu (3) Nyashimba (3), Kipeja (3) na Sagani visima vitatu.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.