ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 12, 2015

WAGANGA 55 WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MWANZA

MWANZA

JESHI la polisi Mkoani hapa limewashikilia waganga wa jadi 55 wanaodaiwa kupiga ramli chonganishi katika msako unaoendelea katika wilaya zote za Mkoa huu.


Waganga hao wa jadi wamekamatwa kutokana na kutuhumiwa kupiga ramli chonganishi zinazosababisha na kuchochea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na wazee (vikongwe).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Valentino Mlowola,alisema waganga hao walikamatwa  Machi 6 mwaka huu, katika msako unaondeshwa na jeshi hilo, kuwasaka waganga wasio na vibali vya kufanya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa kamanda Mlowola alisema waganga hao walikamatwa wakiwa na nyara mbalimbali za serikali ambazo hawazimiliki kihalali na wamekuwa wakizitumia katika shughuli zao za uganga.

“Waganga wasio na vibali,wanaopiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya ya watu wenye ulemavu wa ngozi(albino) ambapo amuaji haya yameleta madhara  makubwa na kuchafua taswira ya nchi yetu." alisema Mlowola.

Katika hali ya kushangaza alisema, mmoja wa waganga hao 55 kati yao wanawake wakiwa 18, alikutwa na madawa ya kulevya aina ya bangi kilo 3, ambayo alikuwa akiitumia kama dawa tiba kwa wateja wake.

kwa mujibu wa Kamanda Mlowola alizitaja nyara walizokutwa nazo kuwa ni ngozi ya samba, mikia ya nyumbu, mikia na pembeza swala, jino la kiboko, korongo, ndege na vinyonga waliokaushwa, yai la mbuni, konokono, kanga na ngozi ya kenge .

Vingine vya ramli chonganishi walivyokutwa navyo waganga hao  ni vibuyu, simbi, visonzo,  sarafu za kale an noti za amani, manyanga, ,fimbo, kioo, vibao, zozo, kengere, njuga, fimbo, kigoda, karatasi za Quran, jiwe mizizi mbalimbali, vyungu, mikuki, mishale, shuka nyeupe, nyekundu na nyeusi.

Alieleza kuwa waganga hao baadhi wamefikishwa mahakamani na wengine bado walikuwa wakiendelea kuhojiwa ambapo alivitaka vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusu mila potofu za imani za kishirikina, kwa kuandika makala za kupinga mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.

“Kwa nafasi yenu nawasihi muielimishe jamii,iachane na mila potofu za imani za kishikirikina kuwa viungo vya binadamu (albino) vinauwezo wa kumtajirisha mtu,bali utajiri unatokana na juhudi za mtu kufanya kazi kwa bidii na si viungo vya binadamu,”alisema Mlowola.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.