ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, May 28, 2014

MALAIKA BAND KUFANYA ZIARA KANDA YA ZIWA.

NA PETER FABIAN, MWANZA.


BENDI ya muziki wa dansi ya Malaika yenye masikani yake jijini Dar es salaam, Mei 30 itakuwa ziarani katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwapagaisha kwa burudani mashabiki wake.

Mratibu wa ziara hiyo, Meneja wa burudani wa Villa Park Resort Ramadhan Maganga alieleza kuwa, ziara ya Bendi hiyo imeratibiwa kwa pamoja na Villa Park Resort ya jijini Mwanza na Alpha Hoteli ya mkoani Geita, ratiba ya ziara hiyo itaanzia Mjini Geita Mei 30 siku ya Ijumaa.

“Wakazi na mashabiki wa Mji huo hakika watashuhudia sauti yenye mvuto ya mwimbaji mahiri Christian Bela na kundi zima la wanamuziki wa Malaika bendi lakini pia watapata fursa ya kuzisikia live nyimbo zao na ufundi wa wapigaji vyombo na wacheza show wakali bila kumsahau Rapa mkali Totoo ze Bingwa pale ndani ya Omega Resort,” alisema.

Maganga alisema kwamba Mei 31 mwaka huu katika ziara hiyo itakuwa zamu ya wakazi na mashabiki wa Jiji la Miamba ya Mawe (Rock City) ambapo bendi ya Malaika itatoa burudani ya uhakika ndani ya Villa Park Resort ambapo Bela ambaye hujiita Rais wa Vijana atafanya makubwa.

“Bela atautambulisha live kwa kuimba wimbo wake mpya unaotamba kwa sasa katika Radio, TV na Kumbi za burudani wa “Nani kama Mama” lakini pia atawashukuru kwa kuwaonyesha mashabiki wa muziki wa dansi Tuzo yake aliyoipata hivi karibuni ya Kilimanjaro Music Award (KMA) 2014 lakini wakiwa Villa watasindikizwa na Bendi ya Super Kamanyola ya jijini Mwanza,” alieleza.

Aidha baada ya jijini Mwanza, bendi ya Malaika itahitimisha ziara yake Kanda ya Ziwa kwa burudani ya kufa mtu katika Mji wa kibiashara na Madini wa Kahama katika Ukumbi wa Social Club ambapo itakuwa ni mara ya kwanza kabisa kufanya ziara yake hiyo kwa Mikoa hii.

Wito wangu kwa wananchi na mashabiki wa muziki wa dansi wasikubali kusimuliwa bali wafike kujionea burudani ya uhakika kutoka kwa wanamuziki wa bendi hiyo ambapo katika maeneo yote watakayotoa burudani mashabiki watalazimika kulipia kingilio cha Sh. 10,000/= tu, ulinzi wa mali utaimalishwa kwa asilimia 100 hivyo hakutakuwa na usumbufu wowote na watoto chini ya miaka 18 hawataruhusiwa kuingia kwenye show hizo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.