ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 27, 2014

ALILAZIMIKA KUKEKETWA ILI ASOMESHWE.

ESTER CHARLES (16) ambaye anasoma kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Rebu iliyoko wilayani Tarime mkoani Mara, alishindwa kujizuia na kudondosha machozi katika ukumbi wa kantini ya jeshi la polisi wilayani Tarime baada ya kueleza masaibu aliyokumbana nayo kwa kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake.

Anapofanyiwa ukeketaji huaminika kuwa mwanamke kamili aliyeondolewa mkosi na ambaye anastahili kuolewa. Wakati anafanyiwa ukatili huo, Esta alikuwa anasoma darasa la saba katika shule ya msingi Rebu, ambapo mara baada ya kukeketwa, anasema alipata maumivu makali ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi.

Anasema alikubali kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba na alikuwa na hamu ya kuendelea na masomo, lakini akapewa masharti na wazazi wake kuwa ili aendelee na masomo lazima akeketwe.

“Sikuwa na jinsi, nilijua ningeenda kukumbana na maumivu makali na kwasababu nilikuwa napenda  shule ilinibidi kukeketwa” anaeleza.
Kutoka maktaba ni moja ya nyenzo za ukeketaji.
UKEKETAJI UNAFANYIKAJE?
Anasema aliamshwa saa 11:30 alfajiri akiongozana na mama yake na wanawake wengine watatu alikwenda kuungana na wasichana wenzake waliokuwa kwenye orodha ya kufanyiwa ukeketaji na kupelekwa mtoni kuogeshwa!

Tuliogeshwa na kupewa maneno ya ujasiri ili tusilie wakati wa kukeketwa “ anasema na kuongeza kuwa Ngariba alilipwa kiasi cha Sh. 10,000/= kwa kila msichana aliyekeketwa (kwa wakati huo). Esta anasema kuna eneo maalum lililotengwa kwaajili ya shughuli hiyo na msichana hushikwa mikono yake kwa nyuma na mama aliyekeketwa.

“Baada ya kufika eneo lile, tulitangaziwa na ngariba kuwa kila mmoja awe na wembe wake, ambao ndiyo alitumia kukeketa” anasema.

Anachokumbuka siku hiyo ni kujikuta tayari amekwisha keketwa huku akitokwa na damu nyingi na maumivu makali. Anasema baada ya kukeketwa, wasichana wote waliwekwa katika uangalizi wa akina mama wasaidizi wakiwemo baadhi ya ngariba, huku wakiwapatia dawa za kienyeji wale wanaovuja damu iliisiedelee kuvuja.

“Nilishindwa kula, nilikunywa uji tu, siku ya pili nilipata maumivu makali baada ya kuamshwa asubuhi kwenda kuogeshwa” anaeleza.
Wakisikiliza kwa makini ni washiriki wa Kongamano hilo lililokuwa mahususi kwa ajili ya kuibua changamoto zilizopo katika jamii kuhusu suala la ukeketaji
Anasema msichana anapotoka jandoni inambidi ashiriki tendo la ndoa na mwanaume ambaye amefanyiwa tohara kama ishara ya kukubali kuwa binti aliyekeketwa kuwa mwanamke kamili na anayestahili kuolewa. Msichana aliyekeketwa huitwa ‘Omonke’.

Anaiomba serikali, asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike, na kwa ngariba wapewe elimu ya kutosha dhidi ya madhara ya ukeketaji.

“Wengi huku Tarime wanafanya hivyo, wakijivunia kukeketwa kutekeleza mila lakini pia ngariba bado hawajapata elimu ya madhara ya ukeketaji, naiomba serikalia na wadau wengine watoe elimu zaidi juu ya madhara ya ukeketaji” anasema na kuongeza kuwa jamii yao huamini kuwa wakimkeketa motto wa kike huleta Baraka katika familia.
NI MADHARA GANI ALIYOKUMBANA NAYO?
Anasema baada ya kukeketwa aliumia sana na aliathirika kisaikolojia ikiwemo kuzomewa nna wasichana wa rika yake ambao hawakuwa tayari kukeketwa.

“Siku niliyokeketwa, nilipata shida sana, nilikuwa na hofu hata wenzangu walikuwa wakinicheka, hata nilipopona nilichukua muda kurudi shule, niliathirika sana” anasema madhara mengine aliyo yapata ni pamoja na kuchanika sehemu zake za siri, kutokana na kukeketwa akiwa na wasiwasi kama atajifungua salama siku za baadaye.

“Mimi nahisi hata wakati wa kujifungua, nitapata matatizo, naomba wazazi wetu wabadilike waanze kwenda na wakati na watambue kuwa wanapotufanyia ukeketaji wanatufanyia ukatili wa kijinsia na kilema cha maisha” anasema.

Anasema kuwa kuna uwezekano wa wasichana wanaokeketwa kupata virusi vya ukimwi kutokana na kukeketwa ba ngariba mmoja, ambaye hukeketa zaidi ya wasichana 50 kwa siku.

Ester anaahidi kuhakikisha wadogo zake Neema na Happy kuwa hawato keketwa kwani yeye kashakuwa mkubwa anayejitambua ana kujua kujieleza.

NDOTO ZA BAADAYE ZA ESTA.
“Nitasomea uandishi wa habari, nitafanya kazi kwa bidii na natamani niwe kama Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba. Nampenda jinsi anavyo wahudumia wanawake” anasema.

Ameiomba serikali kupitia jeshi la polisi kuwakamata mangariba wote wanao husika kufanikisha ukeketaji na kuwafikisha mahakamani, ili sheria ichukuemkondo wake .

Anaitaka jamii ya Wakurya kuendeleza watoto wa kike kitaaluma zaidi badala ya kuwaoza wakiwa katika umri mdogo, na hivyo kushindwa kuhilili kutunza familia.
Kamanda Emmanuel Mkoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime – Rorya, Emmanuel Mkoma anasema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau wengine wilayani Tarime, limeanza kutoa mafunzo ya tohara mbadala itakayo iwezesha jamii kutambua athari za ukeketaji kwa watoto wa kike.
Askari polisi, wanafunzi wa shule za sekondali na tiba ni sehemu ya kusanyiko la washiriki wa Kongamano lililokuwa mahususi kwa ajili ya kuibua changamoto zilizopo katika jamii kuhusu suala la ukeketaji.
Hisia za mmoja kati ya wanafunzi wa kiume na uelewa wa suala la ukatili wa kijinsia na ukeketaji wilayani Tarime mkoani Mara.
Wakisikiliza kwa makini ni wadau wa KIVULINI, Jeshi la Polisi na Wanahabari.
Lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa jamii, ambapo watoto wa kike watapewa elimu ya malezi ya Afya zao itakayo wasaidia wasikeketwe, msisitizo wake ni kuelimisha jamii ione madhara ya ukeketaji na kadri siku zitakavyo kwenda jeshi la polisi linaimani kuwa jamii itaachana na ukeketaji.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.