ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, January 23, 2014

CHADEMA YAIONYA CCM.

Ruvuma/Songea/Tanga. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema kuwa chama hicho kitachukua uamuzi mgumu ikiwa wabunge wa CCM watajikita katika kulinda masilahi yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba kinyume na maoni ya wananchi.

Alisema hayo jana katika Wilaya ya Nyasa na Mbinga kwenye siku ya kwanza ya Operesheni Pamoja Daima. Katika operesheni hiyo, ambapo aliruka kwa helikopta katika sehemu mbalimbali, alihutubia mikutano katika maeneo ya Mbamba Bay, Mbinga, Peramiho, Namtumbo na Songea Mjini.
Akiongozana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Dk Slaa aliwaonya wabunge wa CCM kutotumia wingi wao bungeni kutetea masilahi ya chama chao. “Kamwe wasithubutu kwani Chadema itachukua uamuzi mgumu ambao kwa sasa si vizuri kuutaja,” alisema Slaa.
Alionya akisema ni lazima wabunge watoe maoni ambayo yana masilahi ya wananchi wote na siyo vyama.
Daftari la wapigakura
Katika hatua nyingine, alisema Chadema itasusia kura ya maoni iwapo daftari la wapiga kura halitaboreshwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba.
Alisema kwa sasa chama hicho kinasambaza fomu maalumu nchi nzima kwa ajili ya watu wasio na vitambulisho vya kupiga kura wajiorodheshe.
“Kuna maelfu ya watu waliopoteza vitambulisho vyao vya kupigia kura na wengine wamefikia umri wa kupiga kura lakini Serikali haioni suala hilo kuwa ni muhimu,” alisema.
Alisema uchunguzi wa chama hicho umebaini watu zaidi ya 5,000,000 hawana vitambulisho vya kupigia kura japokuwa tayari wamefikia umri wa kupiga kura.
Ili kuhakikisha Bunge la Katiba linakuwa na manufaa, Dk Slaa aliwataka wananchi kufuatilia mjadala juu ya Katiba Mpya kwa makini ili kuwabaini wabunge wasioitakia nchi hii mema.
Alisema wabunge wa namna hiyo wamepanga kutengeneza Katiba ya viongozi badala ya katiba ya wananchi.
Baadaye katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Matarawe mjini Songea mvua kubwa ilinyesha, lakini wananchi waliofurika hawakujali kunyeshewa badala yake walionyesha shauku ya kuendelea kumsikiliza Dk Slaa. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.