ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 18, 2014

KANUSHO LA Dkt. CHAMI KUHUSIANA NA YALIYO POSTIWA FACE BOOK

Naitwa Cyril August Chami (PhD) Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini na Mjumbe wa NEC-CCM kupitia Wilaya ya Moshi Vijijini.

Nimesikitishwa na kufadhaishwa sana na mtu au watu waliotengeneza akaunti kwa jina langu kwenye  Mtandao wa Kijamii wa Facebook na kujifanya yeye au wao ndio mimi.

Wamepachika hata picha zangu zinazopatikana kirahisi kwa sababu ya majukumu ambayo nimeshawahi kuwa nayo kama Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, na Waziri wa Viwanda na Biashara.

Hilo lenyewe, yaani kutengeneza akaunti kwenye Facebook kwa jina la mtu na kuweka picha zake bila ridhaa yake, ni kosa la jinai.

Lakini ubaya zaidi ni kwamba mtu huyo au watu hao wanawasiliana na wapiga kura wangu kule Moshi Vijijini na walio nje ya jimbo na kuwauliza kero zinazowakabili. Wanawajibu hao wananchi kana kwamba wao ndio mimi. Kwa vile wao sio mimi, majibu yao siyo sahihi. Lakini kwao hilo halina tatizo maana nia yao ni kunichafua.

Wanaenda mbali zaidi na kukitukana Chama changu cha Mapinduzi wakionyesha kuwa mimi ni shabiki na/au sympathiser wa CHADEMA.  Wanatukana wanachama wenzangu wa CCM na kwa maana hiyo, viongozi wangu wa CCM.

Naamini wanajua kuwa nia yao hii ni ovu lakini nawaomba watambue kuwa hawatafanikiwa katika malengo yao kwa sababu mtetezi wangu ni mkubwa kuliko nia hiyo yao.

Siyo siri kuwa asilimia kubwa ya mawasiliano kwenye mitandao yanafanyika kwa anwani feki, hivyo wajue kuwa hata wasomaji wangenishangaa sana kama ningejiundia akaunti ya Facebook,  niweke picha zangu, halafu NIANZE KUWATUKANA VIONGOZI, WANACHAMA NA CHAMA CHANGU CHA MAPINDUZI.

Ifahamike kuwa wakati wao wanawauliza wananchi wangu kero zao kwa Facebook wakiwa kwenye viyoyozi mimi nilikuwa naongea na wananchi hao ANA KWA ANA, siyo tu kuzijua kero zao bali kuzitatua.

Kwa mfano, kuanzia December 20 hadi Januari 17 nimetembelea Kata za Uru Kusini, Uru Kaskazini, Mbokomu, Old Moshi Mashariki, Old Moshi Magharibi, Kimochi, Kibosho Kati, Okaoni, Kibosho Magharibi, Kibosho Mashariki,  Mwika Kaskazini na Mwika Kusini. Nimefika pia TPC kumuonyesha DED wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi sehemu ya kujenga daraja la Samanga litakalounganisha vijiji vya Mikocheni na Chemichemi kwa shs 250 millioni na pia tumetembelea Kata ya Uru Mashariki kukagua barabara inayoanzia Kishumundu Parish hadi Materuni, na ambayo tuko mbioni kui-grade kwa shs 700 milioni na harakati za kuipata hiyo fedha zinakwenda vizuri.

Nimeshiriki fundraising ya kujenga ukumbi wa kisasa Mawella Parish Kata ya Uru Kusini, fundraising ya kujenga bwalo Mangi Meli Sekondari Kata ya Old Moshi Mashariki na fundraising ya kuvijengea uwezo vikundi 16 vya WEKEZA kata za Okaoni na Kibosho Kati. Kabla ya hapo nilishiriki fundraising ya kujenga jengo la utawala Uru Seminari katikati ya Novemba 2013.

Ningekuwa mtumiaji wa Facebook  ningepost events hizi zote na hata kutaja kiasi tulichopata na kiasi cha michango yangu na rafiki zangu.

Hilo sikufanya.

Kwa nini?
Ni kwa sababu asilimia 98 ya wananchi hawa niliowatembelea hawatumii Facebook, nalijua hilo, ndiyo maana nawatembelea kituo kwa kituo nikitambua nikiwasiliana nao kwa Facebook nitapata majibu kutoka kwa asilimia 2 ya wapiga kura, tena walio nje ya jimbo. Na katika kipindi chote hicho sikuweza kwenda kwenye mitandao kwa sababu nilikuwa vijijini kwenye ziara kama Katibu Mwenezi wa CCM Moshi Vijijini, Ndugu Hussein Jamal alivyopost siku chache zilizopita.

Watambue kuwa rekodi yangu ndani ya Bunge, CCM na Serikali inafahamika kuwa mimi si mpayukaji, sina ushabiki na upinzani, na ni kati ya makada wanaoipenda CCM kwa vitendo zaidi kuliko maneno. Kwa maana hiyo wengi wa wasomaji waliosoma hayo wanayonipandikizia wameshaanza kutia shaka kama huyo ndiye Chami wanayemfahamu, na katika hili wako sahihi.

Watambue pia kuwa kama nia yao ni kuniharibia ndani ya CCM na jamii wameshashindwa kwa sababu maneno ya kupandikiziwa kwa wiki moja hayawezi kuaminika zaidi ya rekodi yangu inayofahamika tangu Uru Seminari nilikokuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa miaka 3, Chuo Kikuu cha Dar nilikokuwa Rais wa Wanafunzi Kampasi ya Mlimani, Ikulu nilikokuwa msaidizi wa Rais masuala ya Uchumi, Mbunge, Naibu Waziri na Waziri.

Bila shaka wote nilioishi nao katika maeneo haya na kwingineko watakiri kuwa mimi si mwepesi wa kujisifu, kupayuka na wala si mtu wa matusi kwa mtu binafsi, viongozi wa dini, wa Chama au wale wa Serikali.

Wakati nawaonya waache siasa hizi chafu, nawatahadharisha pia kuwa za mwizi ni arobaini! Ipo siku mtu huyu au watu hawa wataumbuliwa na jamii.

Dr Cyril August Chami.
Mbunge wa Moshi Vijijini.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.