ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 8, 2013

HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA WATOTO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI 1 OCTOBA 2013

Ummy Jamaly Mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA WATOTO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
1OCTOBA 2013

Ndugu watoto wenzangu,                                                                                                                
Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujaalia siku hii ya leo kuwa na afya njema kabisa. Kwa wale watoto wenzangu ambao hali zenu kiafya si njema nakuombeni sana kwa Mwenyezi aweze kuwajaalia afya njema “Amina.”

Ndugu watoto wenzangu,    
Kuanzia leo Alhamis ya tarehe 31/10/2013 nitakuwa nawahutubia ikiwa ni sehemu ya utaratibu wangu mpya wa kuzungumza nanyi watoto wenzangu. Nitajitahidi kila mwisho wa mwezi kutoa hotuba yangu katika sehemu tofauti tofauti kama vile shuleni, kwenye vituo vya watoto, mabaraza ya watoto na hata kwenye ofisi za mashirika ya watoto kama hii leo ambapo natoa hotuba yangu tokea ndani ya ofisi za shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza zilizoko Ghana hapa Jijini Mwanza nchini Tanzania. Shirika hili ndilo ambalo linatuwezesha sisi watoto kuweza kutoa hotuba kupitia program ya “Hotuba ya watoto” Tunashukuru sana shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza kwa kutujali watoto na kutuwezesha sauti zetu kusikika. Pia tunaomba waandishi wa habari muweze kuirusha hewani hotuba yangu ili kuwawezesha watoto wengi waweze kujua kile ambacho ninakihutubia siku hii ya leo. Sina shaka mtatuunga mkono kwa aslimia mia moja.  Nashukuru pia watoto wenzangu kwa kushirikiana nami katika uandaaji wa hotuba hii.

Ndugu watoto wenzangu,                                                    
Kutokana na Takwimu za tafiti mbalimbali zinaonesha ya kuwa asilimia hamsini (50) ya watanzania wote ni watoto na wengi wetu tunafahamu ya kuwa kesho ni leo,je tumejiandaaje na tumeandaliwaje kupokea rasilimali nzuri za nchi yetu? Hakika kila mtu afikirie kwa umakini, apambanue, achambue na afanye maamuzi sahihi, stahiki na magumu kwa ustawi wa nchi yetu hasa katika kutujenga, kutushirikisha na kutuendeleza vyema sisi watoto.

Ndugu watoto wenzangu,
Napenda kuchukua fursa hii kuwaelezea baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakuta watoto wenzetu ambazo zimekuwa ni ukiukwaji wa haki za mtoto. Watoto wenzetu wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kimwili kama vile kupigwa ngumi, mateke na viboko; Ukatili wa kisaikolojia kama vile kutukanwa, kuitwa majina kama vile mbwa, kuku na nguchiro; Ukatili wa kijinsia kama vile kubaguliwa katika kupata elimu na na kazi za nyumbani mfano mtoto wa kiume ndiye anayepewa nafasi ya kusoma, kupumzika na kucheza pia wakati mtoto wa kike akiaachwa nyumbani na kufanyishwa kazi bila ya kupewa muda stahiki wa kupumzika;  na aina nyingine ya ukatili ni ukatili wa  kingono ambapo watoto wenzetu wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa na watu wazima na wenye akili timamu.

Ndugu watoto wenzangu,
Matukio mbali mbali ya ukatili kwa watoto tumekuwa tukiyaskia ama kuyaona yakitokea katika jamii zetu. Mkoani Mtwara mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Newala amepata ulemavu wa akili kwa kupigwa na mwalimu wake kwa madai ya kushindwa kulipia kiasi cha pesa cha shilingi 300 iliyokuwa inachangishwa baada ya kitabu cha shule kupotea. Wakati hayo yakitokea mkoani Mtwara huko Mkoani Dododma mama mmoja mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mchanga. Na hapa Jijini Mwanza, mama mmoja alimmwagia mtoto wake maji ya moto na kumsababishia majeraha na maumivu makali sehemu mbali mbali za mwili wake. Kuna matukio mengi ya ukatili kwa watoto zaidi ya hayo ambayo nimeweza kuyataja yakitokea kila siku katika jamii zetu.

Ndugu watoto wenzangu,
Matukio ya ukatili kwa watoto hayafanywi na miti, wanyama wala wadudu bali yanafanywa na watu wenye akili timamu mbaya zaidi wengi wao ni watu wazima na wenye heshima zao katika jamii. Pia matukio hayo hayafanyiki sehemu ambazo wanaishi mbwa, kuku au paka bali hufanyika sehemu ambazo kuna viongozi wanaotawala, kuna wananchi wanaishi na kuna taasisi zinazoweza kutetea na kumlinda mtoto dhidi ya ukatili.  Ni aibu sana kwa matukio ya ukatili kwa watoto kutokea katika jamii zetu ambazo wanaishi binadaamu na wala si wanyama.
  
Ndugu watoto wenzangu,
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wazazi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuwa tayari kuripoti na kupinga matukio ya ukatili kwa watoto. Na serikali iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaofanya ukatili wa aina yoyote ile ili watoto wote waweze kupata haki zao kwa maslahi ya kujenga Tanzania imfaayo kila mtoto. Kuanzia leo, naomba lugha za matusi kwa watoto zikome, vipigo kwa watoto viishe na matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto tuyazike. Kila kiongozi katika eneo lake, tunamwomba ahakikishe kuwa hakuna mtoto hata mmoja anayefanyiwa ukatili. Na kila mzazi katika familia yake, tunamwomba ahakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili, na kila taasisi katika eneo lake kikazi ihakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili. Tanzania bila ukatili kwa watoto inawezekana, Pamoja tunaweza!
Mungu ibariki Afrika!
Mungu ibariki Tanzania!
Na Mungu wabariki watanzania wote waweze kutulinda sisi watoto dhidi ya ukatili wa aina yeyote ile.

Ahsanteni sana kwa kunsikiliza!

Ummy Jamaly

Mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.