ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 6, 2013

POLISI AVAMIA KAMBI YA ALBINO MISUNGWI, AMNG'OA MENO MLINZI


Matron wa kituo cha walemavu cha Mitindo Judith Mlolwa (mwenyekiti wa CCM wilaya ya Misungwi) 
KATIKA hali ya kushangaza, askari Polisi mmoja wa Kituo cha Misungwi, amevamia shule maalum ya walemavu wa ngozi (albino) na wenye mtindio ya ubongo akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), kwa nia ya kumsaka mlezi wa wanafunzi hao, Judith Mlolwa na kuzua taftrani kubwa. 
Askari huyo, ambaye alionekana kuwa na hasira kwa kile kinachodaiwa kumsaka Mlolwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Misungwi, alisababisha taharuki kubwa ya watoto kukimbia ovyo na kuumia vibaya.

Tukio hilo, lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita, saa 2 usiku shuleni hapo, ambapo askari huyo aliyefahamika kwa jina la Faraji mwenye namba G.3408 alipoamua kutumia nguvu kuingia shuleni hapo.

Katika purukushani hizo, askari huyo alimjeruhi mlinzi wa shule hiyo, Nyamizi Katemi kwa kutumia kitako cha bunduki.

Habari zilizopatikana kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na afisa mmoja ndani ya jeshi la polisi, zimesema Faraji, alifanya tukio hilo akiwa kwenye lindo katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Faraji alipofika shuleni hapo na kusema kuwa anamtafuta Mlolwa na alipojibiwa hayupo aligeuka mbogo na kuanza kutembeza kipigo.

Baada ya askari huyo kujibiwa hivyo, aliingia ndani ya uzio wa shule na kuanza kuwafukuza ovyo ovyo, pasipo na sababu za msingi.

Kutokana na Katemi kumsihi askari huyo, lakini hakumsikiliza ndipo alianza kumshambulia kwa kipigo na kumng’oa meno mawili.

Naye, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kulwa Ng’welo, alisema jana kuwa baada ya kuona vurugu hizo, alipiga simu polisi na askari wawili walifika shuleni hapo na kushindwa kumdhibiti askari mwenzao ambaye wakati huo tayari alikuwa akitamba na kudai kuwa lazima atimize dhamira yake.

“Baada ya taarifa walikuja bila silaha na kushindwa kumdhibiti hata kumsogelea Faraji.

Ofisa mmoja wa polisi, akielezea tukio hilo jana, alidai suala hilo limewaacha mdomo wazi askari wa Misungwi, lakini hakuwa tayari kulielezea zaidi kwa madai kuwa yeye si msemaji wa jeshi hilo.

“Leo (jana) nimefika kwa Kamanda wa Polisi Mkoa na kukutana naye ambapo nimemuelezea kila kitu na alinieleza kuwa alikuwa bado hajapata taarifa za tukio hilo, aliniahidi kuwa nirudi Misungwi na atalifuatilia kwa hatua zote,” alisema Matron Judith.

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alipotakiwa kuelezea tukio hilo, alisema hajapata taarifa na aliahidi kulifuatilia
.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.