ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, July 26, 2012

WALIMU WA MICHEZO MARA WAMPASHAVU BULAYA

Kushoto ni Mbunge wa viti maalum vijana (ccm) Ester Bulaya.

Na Shomari Binda,
Musoma


Walimu wa michezo wa Shule za msingi na Sekondari Mkoani Mara wamemtumia salamu za pongezi Mbunge wa viti maalumu vijana (CCM) Esther Bulaya kwa kuona umuhimu wa suala la kutengewa bajeti nzuri ili kurudisha hadhi ya michezo ya Shule za Msingi na Sekondari Umitashumta pamoja na Umiseta.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati kikao cha Bunge la bajeti ya Wizara ya Habari,Vijana,Utamabuni na Michezo kikiendelea,Walimu hao walisema Mbunge huyo ameliona suala la msingi na kuweza kulizungumzia alipokuwa akichangia katika Wizara hiyo.

Mwalimu wa Michezo wa Shule ya Msingi Kamnyonge A na mwalimu wa timu ya komani ya Umitashumta ya Wilaya ya Musoma Mjini Jedi Kunyenga alisema baada ya kurudishwa kwa michezo hiyo Mashuleni bado imekosa hamasa kutokana na kukosekana fedha za kutosha katika kuendeshea mashindano hayo ambayo yamekuwa yakiibua vipaji kutoka ngazi ya chini.

Alisema katika mashindano ya Mwaka huu kuanzia ngazi ya Shule,Kanda za Wilaya hadi Mkoa yaliyofanyika hivi karibuni yaliendeshwa kwa hali duni na kupelekea kukosa hamasa huku baadhi ya michezo ikishindwa kufanyika kwa kiwango kizuri na kupelekea baadhi ya wanamichezo kushindwa kuonyesha vipaji vyao.

Kwa upande wake Mwalimu wa michezo katika shule ya Sekondari Mmazami iliyoko Wilaya ya Butiama Mugisha Garibona alisema hata kwa upande wao hufikia hatua walimu kuchangishana pesa kwa kila Shule ili kuweza kufanikisha mashindano hayo kutokana na kukosa bajeti ya kuendeshea.

Alisema mashindano ya Wilaya waliyaendesha kwa ukata mkubwa na hata ilipofikia wakati wa kupeleka timu ya Mkoa katika mashindano ya Taifa Kibaha Mkoani Pwani iliwalazimu kupitisha tena bakuli ili kuweza kuwapeleka vijana kushiriki mashindano hayo ya Kitaifa.

Kwa pamoja Walimu hao walidai Mbunge Bulaya aliona mbali katika kuzungumzia suala la bajeti ya michezo mashuleni ili kuweza kuleta ufanisi katika mashindano hayo ambayo ni ndio chimbuko la kuibua vipaji vya michezo mbalimbali na badae kulitangaza Taifa kupitia michezo

Katika kuchangia Wizara hiyo ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Bulaya aliitaka Serikali kuweka bajeti kwa ajili ya michezo kwa shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISETA).

Alisema pamoja na Serikali kurudisha michezo mashuleni lakini haifanyiki kwa ufanisi kutokana na ufinyu wa bajeti inayotolewa kwa michezo hiyo licha ya serikali kuamua kuirudisha mara baada ya kuifuta kipindi cha nyuma.

Mbunge Bulaya alitaka kujua Serikali imejipanga vipi kibajeti kuhakikisha inarudisha michezo mashuleni kama ilivyokuwa hapo zamani.

Akimjibu Mbunge huyo Naibu Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Amos Makalla alisema ni kweli ni kweli Serikali ilirudisha michezo shuleni na kumuomba Bulaya kupitisha bajeti ya Wizara yake ambayo pia imelenga kuendeleza michezo mashuleni.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.