ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 20, 2012

MENEJA MELI ILIYOZAMA ZANZIBAR AKAMATWA : TAIFA LAOMBOLEZA


Bendera zikipepea nusu mlingoti katika jengo la makao makuu ya CCM mkoani Mwanza ishara ya maombolezo.

VIFO VYA FIKIWA WATU 63, SERIKALI YATANGAZA SIKU TATU MAOMBOLEZO
 Waandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Omari Hassan Mnkhon ambaye ni Meneja wa boti ya Mv Skagit, kwa ajili ya mahojiano baada ya kubainika kwamba kumekuwa na kasoro za kumbukumbu katika taarifa za hiyo.Wakati Jeshi hilo likimshikilia meneja huyo, hadi jana jioni saa 10:30, vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kupata maiti 63, huku 29 kati yao ikiwa imetambuliwa majina namba za tiketi na sehemu wanakotoka marehemu.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa meneja wa boti Mkoa wa Dar es Salaam, anashikiliwa ili kuweza kusaidia jeshi la polisi kupata taarifa za kina kuhusu za meli hiyo.

Kova alisema tukio hilo linagusa maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam ambako safari za meli hiyo huanzia na kuongeza kwamba, wanamshikilia meneje huyo baada ya kukosekana taarifa muhimu juu ya safari za boti hiyo.



Wananchi wakiwa kwenye foleni katika viwanja vya Maisara mjini unguja Zanzibar jana kwa ajili ya kwenda kutambua miili ya ndugu zao waliofariki kwenye ajali ya meli MV Skygat, iliyozama eneo la chumbe Zanzibar juzi. Picha na Fidelis Felix

Maiti zilizotambuliwa
Hadi saa 10 jioni jana, maiti 63 zilikuwa zimepatikana na watu 145 kuokolewa wakiwa hai. Hata hivyo kati ya maiti hizo zilizopatikana, matiti 34 zilichukuliwa na ndugu zao.

Baadhi ya maiti waliotambuliwa pamoja na umri wao na maeneo wanayoishi katika mabano ni Anita Emanuel (42, Kibamba -Dar es Salaam), Rukiya Issa Muombwa (miezi 2, Meli nne –Fuoni Zanzibar ), Halima Ali Khamis (23, Mtopepo- Zanzibar), Kolin Krispin (miezi 9, Kunduchi - Dares Salaam) na Rahma Ali Abdalla (miaka 52, Mfenesini - Zanzibar).

Maiti wengine ni Said Jumanne Masanja (miaka 9, Nzega Tabora), Sauda Abdalla Omar (22, Ole Pemba), Said Juma Said (36, Arusha), Amina Abdalla Tindwa, (miezi 6, Fuoni), Halima Ramadhani Kilimo, (53, Morogoro), Khadija Omar Ali (58), Amina Hamir Bakari (39, Chukwani - Zanzibar), Mwanahamisi Mshauri (42, Kibandamaiti), Ali Hamdu Othman (35, Mkwajuni) na Mohamed Said Salum (40, Magomeni Mikumi - Dares Salaam).

Wengine ni Amina Ahmed Ramadhani (21, Michenzani zanzibar ), Mgeni Juma Halfani (25, Daraja Bovu), Khadija Rajab Kibune (22, Fuoni), Maua Ramadhani Feruzi (29, Mwembeladu), Hussein Ali Khamis (4, Mwanakwerekwe) na Sabiha Heri Mbarouk (25, Mgeleme, Chakechake-Pemba).

Pia wamo Halima Ali Mohamed (35, Kiwengwa- Zanzibar), Asia Juma Khamis (29, Kiembe Samaki), Yusuf Hasan Yusuf (7, Chamanzi, Dar es Salaam), Batuli Abrahmani Amir (20, Jang'ombe), Fatma Said Sultani (54, Msasani Dar es Salaam), Juma Jafari Shajak (Miezi 6, Kimaneta - Tanga) na Mohamed Ali Ngombe (41, Buguruni - Dares Salaam).



Serikali yatangaza siku
tatu za maombolezo

Kufuatia msiba huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi Julai 21 mwaka huu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na shughuli zote zinazoambatana na sherehe na burudani zimefutwa kwa muda huo lakini kazi na shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida

Nayo Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ilitangaza siku tatu za maombolezo kufuatia msiba huo mkubwa uliolikumba taifa.

Rais Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na huduma za matibabu kwa majeruhi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa Bungeni Mkoa wa Dar es Salaam ndio umepewa jukumu la kushuhulikia suala hilo. Alisema kwa sasa mkoa Umepanga kutoa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhi mili ya watu waliofariki katika ajali hiyo. “Watu wote ambao wanajua kuwa ndugu zao walisafiri na meli hiyo wafike katika bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya utambuzi,” alisema na kuongeza kuwa ambayo haitatambuliwa Serikali itachukua jukumu la kuizika.

EU yatoa ndege ya uokoaji
Katika kuonyesha kuguswa na ajali hiyo, Umoja wa Ulaya (EU) umetoa ndege maalum kusaidia juhudi za utafutaji na uokoaji katika eneo la ajali.

Balozi wa Uingereza hapa nchini Diane Corner aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar kuwa wameamua kutoa msaada wa ndege hiyo ambayo iliwasaili Zanzibar usiku wa kuamkia Julai 19, kitokea katika visiwa vya Ushelisheli. “Nawapa pole watu wa Zanzibar kwa msiba huu, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana, hasa nilipoziona maiti saba za watoto wadogo. Moyo wangu umeumia sana,” alisema huku akibubujikwa machozi.

Wabunge wachangia maafa
Katika hatua nyingine, wabunge wote watakatwa posho ya siku moja kuchangia maafa ya kuzama kwa boti hiyo huku Bunge likiahirishwa kwa siku moja kuomboleza maafa hayo.

Posho hizo za wabunge zitawezesha kupatikana kwa Sh24.6 milioni kutoka kwa Wabunge wa sasa 352 ambao kila mmoja atachagia Sh70,000.

Wakizungumza baada ya ajali hiyo, baadhi ya wabunge waliitupia lawama Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kwa kile walichodai kuwa ilishindwa kutoa taarifa ya tahadhari kwa watumiaji wa usafiri wa majini.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema mamlaka hiyo inabeba lawama kwa kushindwa kutoa ushauri kwa vyombo husika na badala yake wanafanya kazi ya kutabiri mvua tu.

Mbali na Mamlaka ya Hali ya hewa, lakini mbunge huyo alitaka pia wakaguzi wa vyombo vya majini kuwajibika kwa kushindwa kukagua uimara wa vyombo hivyo.

TMA watoa kauli
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Hamza Kabelwa alisema kuwa, kupitia ofisi yao iliyopo bandarini Dar es Salaam walitoa taarifa kwenye vyombo vya usafiri wa majini juu ya upepo mkali uliokuwa ukivuma baharini kwa kasi ya kilometa tatu kwa saa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi. “Tulipogundua hali hiyo tulitoa taarifa kwa wahusika wa vyombo vya usafiri wa majini tu,” alifafanua Dk Kabelwa.
Meli ya Skagit ilitengenezwa mwaka 1989 nchini Marekani na ilikuja nchini 2008.
SOMA ZAIDI GAZETI LA MWANANCHI

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.