ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 13, 2011

KOFIA YA JESHI LA JWTZ YAFUNGA BARABARA

Leo jioni kwa mara nyingine, Jijini Mwanza kumetokea vurugu iliyopelekea wananchi kufunga barabara kuu ya Mwanza - Musoma kwa kutumia magogo, matawi na kuchoma matairi.

Kizuizi kikimaliziwa kuondoshwa barabarani.
Sekeseke limekuja tu mara baada ya askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa katika Operesheni maalum inayoendeshwa ya kukamata pikipiki zenye makosa ya usalama wa barabarani, kumshambulia kwa kipigo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Askari huyo wa JWTZ (pichani aliyekifua wazi), ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, alikumbwa na mkasa huo, baada ya askari polisi kukamata pikipiki yake kwa lengo la kukagua uhalali wa kuendeshwa barabarani.

Hata hivyo, wakati askari polisi wakimhoji huku pikipiki nyingine takribani kumi na tano zikiwa zimekamatwa, askari huyo wa JWTZ alimgeukia mmoja wao na kumuamuru kuvua kofia aliyokuwa amevaa kwa madai kwamba, ni mali ya JWTZ.

Amri ya askari huyo wa JWTZ ilipingwa na askari polisi, ambao walifura kwa hasira nakuanza kumpa kipigo.

Kitendo hicho kiliwaudhi wananchi waliokuwa wakifuatilia tukio hilo wakidai kuonewa mara kwa mara na askari hao, ambao waliingilia kati na kuanza kuwashambulia askari hao kwa mawe.

Askari hao walipoona wamezidiwa, walikimbilia katika kituo cha polisi cha Market na wananchi hao waliendelea kuwashambulia kwa mawe.

Vurugu hizo zilizotokea katika eneo la Nyakato, zilisababisha Barabara ya Musoma kufungwa kwa muda hali iliyo sababisha hata msafara wa mkuu wa mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro ulio kuwa ukitokea wilayani Magu kwenye maonyesho ya Saba saba nao pia kujisitiri kituoni hapo kuhofia usalama.

Kutokana na vurugu hizo, askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika na kuanza kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu ya machozi huku wakikamata baadhi ya watuhumiwa walioonekana kuhusika na sakata hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro, alithibitisha kuwapo operesheni ya kukamata pikipiki na kusisitiza kuwa zoezi litaendelea.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.