ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, May 17, 2011

MWANARIADHA WANJIRU AOMBOLEZWA

Wanariadha mashuhuri duniani pamoja na wapenzi wa riadha wamekuwa wakielezea masikitiko yao kufuatia kifo cha ghafla cha bingwa wa Olimpiki wa mbio za Marathon, Samuel Wanjiru wa Kenya.

Mwanariadha huyo wa Kenya alifariki dunia Jumapili usiku nyumbani kwake akiwa na umri wa miaka 24. Polisi wameeleza kuwa alianguka baada ya kuruka kutoka kwenye baraza la ghorofa ya kwanza nyumbani.

Wamesema mwanariadha huyo alikuja nyumbani usiku akiandamana na mwanamke mwingine, na baadaye mke wa Wanjiru- Triza Njeri alikuja akawakuta chumbani, na kwa hasira akafunga mlango wa chumba hicho huku akimwambia mumewe anakwenda kuwaarifu polisi..


Triza njeri (left), Ms Judy Wambui (centre) and international atlete Mary Wacera.
Haijabainika ikiwa Wanjiru aliruka nje kujiua, au kumfuata mkewe, au kwenda kufungua mlango wa chumbani. Polisi waliwahoji wanawake hao wawili kubaini kilichotokea.

Mwezi Desemba Wanjiru alishtakiwa kwa kutishia kumuua mkewe, kumiliki bunduki kinyume cha sheria na pia kumjeruhi mlinzi wa nyumbani.

Baada ya mkewe kuondolea mbali kesi inayomhusu walirudiana, na Wanjiru alitazamiwa kufika mahakamani kuhusiana na shtaka la kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Sammy Wanjiru alikuwa na umri wa miaka 21 aliposhinda medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 mjini Beijing , China, na akawa Mkenya wa kwanza kushinda dhahabu kwenye mbio za marathon za Olimpiki.

Chipukizi huyo aliibuka mwaka 2004 wakati huo akiwa na umri wa miaka 18 , aliposhinda mbio za marathon za Fukuoka nchini Japan.

Baada ya kushinda taji la Olimpiki, mwaka uliofuatia alishinda mbio za London na pia Chicago. Mwaka jana alitetea taji la Chicago.

Ilitazamiwa na wengi kwamba mwanariadha huyo angeweza kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za Marathon ambayo kwa sasa inashikiliwa na Haile Gebreselassie wa Ethiopia.

Haile ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo hicho.

''Najiuliza ikiwa sisi kama jamii ya wanariadha tungeweza kusaidia kuepusha tukio hilo.'', alisema Haile kwenye mtandao wa Twitter.

Katibu mkuu wa chama cha riadha nchini Kenya David Okeyo amesema kifo cha Wanjiru ni pigo kubwa kwa Kenya.

'' Alikuwa mwenye furaha na tulitazamia angevunja rekodi ya dunia ya mbio za marathon hivi karibuni'', alisema Okeyo.

Bingwa wa zamani wa dunia Paul Tergat pia kutoka Kenya amesema nchi hiyo imepoteza mwanariadha chipukizi mwenye kipaji.

'' Ni habari za kusikitisha sana, na ni pigo. Alikuwa mwenye umri mdogo na alikuwa na nafasi ya kukimbia kwa miaka mingi. '' alisema Tergat.

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amesema kifo cha Wanjiru ni pigo kubwa kwa matazamio ya Kenya ya kushinda medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka ujao mjini London

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.