ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, May 11, 2011

MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA HATIMAYE YAFANYIKA LEO MWANZA / SABABU ZATAJWA

Kutoka mkoani Mwanza inatajwa kuwa kwa mwaka uliopita 2010 takribani watu wapatao 309,163 wameugua malaria, huku idadi ya watu 1,063 wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakitajwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.Mganga mkuu Dr.Mmasi.
Hayo yamebainishwa leo katika Taarifa fupi ya maadhimisho ya siku ya malaria duniani yaliyokwenda sambamba na upimaji bure wa malaria uliyofanyika kwenye viwanja vya Ghand Hall jijini Mwanza nakusomwa na Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dr. Meshack Massi.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa wakazi wa Mwanza wako katika hatari kubwa kupata malaria kutokana na kuwa katika ukanda wa mazalio ya mbu waenezao ugonjwa wa malaria kwa vile sehemu kubwa ya ardhi inatuamisha maji kwa muda mrefu, kupata mvua za vuli na masika kwa mwaka sambamba na eneo lake kubwa la ardhi kuzungukwa na mwambao wa ziwa Victoria.

Wananchi kwa zamu wasubiri kupima malaria ndani ya Ghand hall Mwanza.
Jamii imepata athari kubwa kutokana na ugonjwa wa malaria ikiwa ni pamoja na kudhoofu kwa afya ambayo ni nguvu kazi kwa watu wake ambayo imesababisha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo na kuwa chanzo cha umasikini ikiwa ni zao la kushindwa kutekeleza majukumu ya shughuli za kila siku za maendeleo.

Ili kupata dozi kwa tiba ya malaria, vipimo vya uzito muhimu.
Dr. Massi amezitaja baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mapambano dhidi uganjwa wa Malaria kuwa ni pamoja na jamii kuchelewa kwenda kwenye vituo vya tiba kupatiwa matibabu pindi wanapougua (delay in health seeking behavior), baadhi ya wagonjwa kutozingatia ushauri wa matibabu sahihi ya malaria unaotolewa na wataalam wa afya na imani potofu ya matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu vya muda mrefu.

Kujiandikisha.
Aidha halmashauri ya jiji la Mwanza imejiwekea malengo kupunguza maambukizo ya ugonjwa wa malaria toka asilimia 36.1 hadi 25 na kupunguza kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka 5 vinavyotokana na malaria kutoka 8/1000 hadi 5/1000 kwa mwaka.

Upimaji.
Shughuli zitakazo fanyika kufikia malengo hayo ni pamoja na kuhamasisha matumizi endelevu ya vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu vilivyogawiwa ngazi ya kaya, kuhamasisha usafi wa mazingira, kuhamasisha jamii kuwahi kwenye vituo vya tiba ili kupata matibabu sahihi ya ugonjwa wa malaria na kuwahimiza wanawake wajawazito kuwahi kliniki ili kupata kwa wakati dawa ya SP inayowakinga dhidi ya maambukizo ya malaria.

SABABU YA JIJI LA MWANZA KUFANYA MAADHIMISHO HAYO LEO
Siku ya malaria duniani huadhimishwa tarehe 25 April ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa tarehe 29 April mkoani Arusha baada ya kuahirishwa kutokana na kuangukia siku ya jumatatu ya pasaka na katika jiji la Mwanza maadhimisho hayo yamefanyika leo tarehe 11/05/2011 kutokana na sababu zilizotajwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.