ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 3, 2011

Mbowe na Kikwete USO KWA USO.

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe jana alikutana uso kwa uso na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni mara ya kwanza tangu chama hicho kilipotangaza kutotambua ushindi wa Kikwete uliompa fursa ya kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka mitano kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana.Tukio hilo la aina yake kutokea tangu kuanza kwa mwaka huu, liliwakutanisha Mbowe na Rais Kikwete katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo walisalimiana kwa kupeana mikono.

Mbowe na Kikwete walikutana uso kwa uso ikiwa ni siku 85 tangu Mbowe alipowaongoza wabunge wa chama chake kususia hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 10, Novemba 18 mwaka 2010 kutokana na msimamo wa chama chake kutotambua matokeo ya urais.

Mwaka jana, Mbowe alitangaza chama chake kutotambua matokeo ya rais huku akitoa madai mbalimbali kuhusu taratibu zilizotumika kumwingiza kiongozi huyo madarakani.

Katika tukio la kupiga picha za pamoja ndipo Mbowe alikutana uso kwa uso na Rais Kikwete ambapo walisalimiana kwa kupeana mikono na kupiga picha pamoja huku wote wakiwa na tabasamu pana.

Alipotafutwa na gazeti la Mwananchi (wanyetishaji wa inshu hii) ili kuzungumzia tukio hilo, saa kadhaa baada ya kumalizika kwa sherehe hizo, Mbowe alisema alikwenda katika sherehe hizo kwa kuwa zilikuwa ni za mahakama na kwamba hata kungekuwa na tofauti gani kusingemzuia yeye kusalimiana na Kikwete.

"Sherehe zile si zangu wala Rais Kikwete hivyo siwezi kuwa na chuki na mahakama, ni 'Birthday' ya Mahakama yenyewe ni mhimili wa dola," alisema Mbowe.

Mbowe alisema kuwa katika maadhimisho hayo alialikwa kama mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Mbowe alisema kuwa madai waliyotoa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana haikuwa na maana kwamba hawaitambui Serikali wala kutaka Rais Kikwete ang’oke madarakani.

Alisema kuwa mambo mawili kati ya matatu yaliyokuwemo katika dai lao yameshaanza kupatiwa ufumbuzi kwa namba moja au nyingine ambayo ni katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.


RAIS AZUNGUMZIA IMANI YA WANANCHI KWAKE:
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekosa imani naye kutokana na msimamo wake wa kukataa kuingilia uhuru wa Mahakama wanapomtaka atengue maamuzi mbalimbali ya korti.
Kikwete alikuwa akizungumzia uwelewa wa wananchi juu ya sheria mbalimbali na nafasi ya Mahakama ambapo alisema kuwa wananchi hawana budi kufahamu jinsi Mahakama inavyofanya kazi.

Rais alitoa wito kwa Mahakama kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari katika kutoa elimu kuhusu sheria.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.