ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, January 30, 2011

WAMACHINGA WAFANYA VURUGU MWANZA.

JIJI la Mwanza jana lilikumbwa na machafuko baada ya machinga kufanya vurugu na kuandamana wakipinga kuondolewa kufanya biashara katika maeneo ya mjini kati. Vurugu hizo zilisababisha kufungwa kwa maduka katika maeneo mbalimbali mjini hapa, kuvunjwa vioo vya magari, maduka na baadhi ya barabara kutopitika kwa muda huku kituo kidogo cha Polisi Pamba, kikinusurika kuvamiwa na kuchomwa moto.MKUU WA MKOA WA MWANZA ABBAS KANDORO AKIZUNGUMZA NA WAANDAMANAJI HAO KUPITIA GARI LA FFU, KULIA MWENYE SHATI YA BLUE NI MWENYEKITI WA WAMACHINGA MZ.
Pamoja na vurugu hizo, serikali mkoani Mwanza imewataka wafanyabiashara hao kuheshimu sheria na kanuni za mipango miji zilizowekwa pia maafikiano yaliyofikiwa baina ya viongozi wao, uongozi wa mkoa na halmashauri ya jiji hilo .

PATASHIKA MITAA YA MIRONGO.
Vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa sita, zilianza saa tatu asubuhi baada ya mgambo wa jiji na askari wa kutuliza ghasia kuwatawanya wafanyabiashara hao katika maeneo ya Makoroboi, Mission na Soko Kuu.

WAMACHINGA WAKIKUSANYA BIDHAA ZAO.
Kutokana na hali hiyo, machinga walijikusanya na kuanza kuvamia maduka, magari kabla ya kuandamana saa 4:38 asubuhi hadi katika jengo la ofisi za Halmashauri ya jiji la Mwanza wakishinikiza kutoondolewa katika maeneo hayo.

Nje ya jengo hilo , waliweka vizuizi vya mawe katika barabara zote zinazoingia jiji na kulazimisha pikipiki na magari yaliyokuwa yakipita kurudi yalikotoka huku wakiwa na chupa za maji ya kunawa kwa ajili ya kujikinga na moshi wa mabomu iwapo polisi wangewafyatulia mabomu ya machozi.

Hali hiyo ilisababisha polisi wa kutuliza ghasia na makachero kuweka ulinzi mkali katika lango kuu la kuingilia jiji hadi viongozi akiwemo Mkurugenzi wa jiji Wilson Kabwe na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro walipofika na kufanya mazungumzo na viongozi wa machinga hao.

Baada ya mazungumzo hayo, Kandoro aliwaambia machinga kuwa hapingani na sheria na kanuni za mipango miji kwa kuruhusu machinga wafanye biashara katika maeneo waliyoruhusiwa, isipokuwa wafuate masharti waliyopewa katika maeneo ya Makoroboi, Mirongo, Vitunguu Soko Kuu na Mlango Mmoja.

AJALI KATIKA PILIKA ZA KUNUSURU BIASHARA.
Baada ya kuondoka katika ofisi za halmashauri hiyo, machinga waliingia mitaani tena na kuanza vurugu wakivamia maduka na kuvunja vioo kwa madai kwa wafanyabishara wengine, hawatafanya biashara.

Sambamba na kuvamia maduka, walijiandaa kwenda kuvamia Kituo cha Polisi Pamba kwa lengo la kukichoma moto kwa kutumia matairi ya gari kabla ya polisi waliokuwa doria kuwawahi na kuwadhibiti, ambapo walitupa matairi ya moto katika barabara ya Pamba jirani na kituo hicho.


Awali, katika vurugu hizo magari T. 541 BHN aina ya Toyota Carina, T. 352 ALF, T.234 ASA na lori aina ya FIAT lenye namba T. 988 AGM, yalipigwa mawe na kulazimishwa kutopita jijini ambapo gari hilo lilivunjwa kioo cha pembeni mbele. Gari lingine lililovunjwa kioo cha nyuma katika eneo la Rwagasore ni T. 400 AHT aina ya Toyota Land Cruiser mali ya mfanyabishara maarufu Mkeshi Vunjabei ambaye baadaye saa 7:52 mchana walivamia duka lake, lakini waliwahiwa na polisi.

Barabara zilizokumbwa na vurugu hizo na kutopitika kwa muda huku wafanyabiashara wengine wakifunga maduka yao kuepuka vurugu hizo ni Nyerere, Rwagasore, Rumumba, Uhuru, Makoroboi na Liberty. Hadi jana jioni, vurugu zilikuwa zikiendelea katika baadhi ya maeneo na kufanya mji wa Mwanza kuwa kimya kutokana na shughuli kusimama, hata hivyo vurugu hizo hazikuwa kubwa.

Tupe maoni yako

5 comments:

  1. hapo ndipo utajua utamu wa serikali na jamii yake full kumwaga damu

    ReplyDelete
  2. hapo ndipo utajua utamu wa serikali na jamii yake full kumwaga damu

    ReplyDelete
  3. hapo ndipo utajua utamu wa serikali na jamii yake full kumwaga damu

    ReplyDelete
  4. hapo ndipo utajua utamu wa serikali na jamii yake full kumwaga damu

    ReplyDelete
  5. hapo ndipo utajua utamu wa serikali na jamii yake full kumwaga damu

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.