ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, January 6, 2011

HABARI ZILIZOVUNJIKA MUDA HUU: CHADEMA YAULA UMEYA NA UNAIBU MEYA JIJI LA MWANZA. WAJIBEBA KWA MBELEKO YAO WENYEWEee!!.

Hatimaye jiji la Mwanza leo limepata Meya wake mpya baada ya kura za Madiwani wapatao 32 kupigwa nazo kuhesabiwa na mwisho wa mchezo diwani wa kata ya Nyakato bw. Josephat Manyerere wa CHADEMA kutangazwa kuwa ndiye meya mpya wa jiji la Mwanza. Akitangaza matokeo ya umeya Mwanza, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni mkurugenzi wa jiji bw. Wilson Kabwe amemtaja Bw. Stanslaus Mabula (CCM) kuwa amepata kura 15, na Bw. Josephat Manyerere (CHADEMA) akiibuka mshindi kwa kupata kura 17.

Huyu ndiye meya mpya wa jiji la Mwanza kupitia CHADEMA Bw.Josephat Manyerere(kulia) akipongezwa na mbunge wa Nyamagana Mh.Wenje, na kwa chati pembeni ni diwani wa Mwaloni Kirumba Bw.Novat Manoko.

Mara baada ya mchakato wa kumpata Meya kumalizika na mshindi kutajwa, ungwe iliyofuata ikawa ni kumsaka Naibu Meya ambapo kulikuwa na wagombea wawili nayo matokeo yakataja kuwa diwani Charles Marwa Chichibela (pichani mwenye suti) kutoka CHADEMA ameibuka kidedea kwa kuzinyakua kura 17, dhidi ya 15 za Daudi Mkama wa CUF.

Mbunge wa Kigoma kaskazini Mh.Zitto Kabwe (mwenye leather coat) akifuatilia kwa umakini uchaguzi huo.

Kanuni na taratibu zote za sheria zilizingatiwa ndani ya ukumbi wa uchaguzi huo, pichani ni moja kati ya hatua za kuhesabu kura.

Moja baada ya nyingine hapa ni katika mchakato wa kuhakiki matokeo ndani ya ukumbi wa mikutano, ofisi za jiji la Mwanza Uchaguzi kumpata Meya na Naibu wake.

Hii ndiyo taswira ya sehemu ya safu ya madiwani 30 na wabunge wao wawili kufikisha idadi ya wapiga kura 32 waliohusika na mchakato huo.

KURA HAZIKUTOSHA: Kushoto ni Daudi Mkama aliyegombea nafasi ya naibu meya kupitia CUF na Stanslaus Mabula (CCM) aliyegombea nafasi ya Umeya.

Wafuatiliaji wa uchaguzi na nidhamu ya hali ya juu.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini mh.Zitto Kabwe (kushoto) na mbunge wa Nyamagana mh.Wenje wakipongezana.

Fair Play:- Hapa ni kati ya Wenje na Mabula.

Mbunge wa wilaya ya Ilemela Mh.Hainess Samson akipongezwa na Zitto.

MAHOJIANO NA Z.KABWE :-"Kwanza nawapongeza madiwani wa Mwanza kwa maamuzi haya mazuri waliyoyafanya. Pili kwa lile lililotokea jana sisi kama CHADEMA Tunalaani kwa nguvu zote ubabe na matumizi ya ovyo ya nguvu za dola. Tunalaani jeshi la polisi kuendelea kukubali kutumiwa na wanasiasa katika kuficha udhaifu wao wa kisiasa na kiuongozi. Jeshi la polisi limeendelea kuvunja sheria kwa kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara, jeshi la polisi limegeuka kuwa watoa vibali! Watawala wajue kuwa hakuna nguvu ya risasi itakayoshinda nguvu ya umma inayotaka mabadiliko, na wala CCM haitaweza kulazimisha kubaki madarakani kwa nguvu ya risasi. CHADEMA tutaendelea na juhudi za kuhamasisha wananchi kudai haki zao za kidemokrasia ikiwemo kuwajibisha viongozi waliowachaguwa kuwaletea maendeleo"

Tupe maoni yako

1 comments:

  1. tunashukuru mungu zoezi limeenda salama. Ha ha haaa naona CUF walifunga ndoa na CCM mwanza

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.