ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, May 11, 2010

BGML YAZINDUA GAZETI LA JAMII:

- Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja mstaafu Bahati Matala,(kushoto), akifungua utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa gazeti la jamii,"BUNAKOBA" linalotolewa Na Mgodi wa Dhahabu Bulyanhulu, (BGML),kulia ni Afisa Mawasiliano wa BGML, Basil Mbakile na katikati ni mmoja wa viongozi wa kata ya Bugarama wilayani Kahama. Uzinduzi Huo ulifanyika Jumamosi tarehe 8 Mei 2010.

HABARI KAMILI:
Serikali imetoa changamoto kwa jamii inayoishi jirani na mgodi wa Bulyanhulu kujenga utamaduni wa kujisomea ili kupanua wigo wao wa uelewa.
Changamoto hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja mstaafu Bahati Matala, wakati akizindua gazeti la jamii la BGML linaloitwa”BUNAKOBA” mnamo Mei 8 2010.
Meja Matala amesema gazeti hilo ni kiungo muhimu katika kutoa habari mbalimbali kati ya mgodi na jamii na kwamba ni njia ya kuimarisha mahusiano mazuri baina ya pande hizo mbili.
“Ninatoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi za BGML katika kubadilishana habari za kijamii, kiuchumi na utamaduni zinazohusu jamii na kuitumia fursa hii kujielimisha”, alisema Mkuu wa Wilaya.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi, Afisa Mawasiliano wa BGML, Basil Mbakile, alisema uamuzi wa kuanzisha gazeti la jamii ulifikiwa baada ya kutambua umuhimu wa kufikisha habari mbalimbali kwa jamii inayozunguka mgodi hasa zile zinazohusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na mgodi kwa jamii na pia wananchi wenyewe kutoa habari zinazowahusu hivyo basi kuboresha mawasiliano baina ya jamii na mgodi wenyewe.
“Tunaamini kwamba gazeti hili la jamii litasaidia kuwapatia wananchi habari sahihi juu ya shughuli za uendeshaji mgodi pamoja na miradi ya maendeleo kwa jamii, ambazo mara nyingi zimekuwa haziwafikii wananchi kwa usahihi,” alisisitiza Basil.
Alisema mbali ya kukusanya na kuandika habari za vijijini na zile zihusuzo mgodi, Idara ya Mawasiliano inaandaa utaratibu wa kushirikiana na vyombo vingine vya habari nchini, wizra, taasisi, mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, (NGO), na wengineo katika tasnia ya habari ili kuhakikisha gazeti letu linapanua wigo wake wa habari na pia wananchi wanapata taarifa muhimu zinazowagusa.
Jina “BUNAKOBA” linamaanisha “Watu Watafutaji” kwa lugha ya Kisukuma. Gazei la BUNAKOBA linatayarishwa kwa pamoja na Idara ya Mahusiano na Jamii na Idara ya Mawasiliano ambalo litatolewa kila baada ya miezi minne na kugawiwa bure kwa wananchi.


- Pichani ni baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa gazeti hilo wakijisomea nakala ya kwanza ya gazeti.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.